.

.
TZ WAKA BLOG TUNAKUTAKIA HERI YA MWAKA MPYA 2016, MWAKA HUU UWE WA BARAKA NA MAFANIKIO KWAKO | KUTANGAZA NA BLOG HII WASILIANA NASI KUPITIA 0716 979 939 AU BARUA PEPE tzwakablog@gmail.com

Serikali yatakiwa kuimarisha Usimamizi wa Viwanda kuepuka uchafuzi wa Mazingira


VIWANDA vinavyozalisha bidhaa mbalimbali Jijini Dar es Salaam na maeneo 
mengine nchini vimelalamikiwa kwa kutoweka mazingira salama kwa watu 
wanaoishi maeneo jirani.
Baadhi ya malalamiko hayo ni pamoja na viwanda vilivyopo katika eneo la Boko CCM, Basihaya Jijini Dar es Salaam, wawekezaji wa China wanaotafuta madini Wilayani Mkuranga mkoani Pwani na Kiwanda cha Saruji Songwe ambacho kiko jirani na Uwanja wa Ndege Songwe ambacho kinalalamikiwa kwa tatizo la vumbi kuathiri usalama wa abiria wanaofika katika uwanja huo pamoja na wakazi wanaozungukwa na eneo hilo.
Viwanda hivyo huchafua mazingira  kwa kutiririsha maji machafu na kutumia baruti kupasua miamba katika maeneo hayo. Wakazi wa maeneo ya Boko CCM wameeleza kuwa wamepata shida hiyo kwa muda mrefu na kwamba hakuna mikakati madhubuti ya kudhibiti hali hiyo ambayo ni pamoja na kulipwa fidia wananchi ambao wameathiriwa na uwepo wa viwanda hivyo.
Hata hivyo, kilio cha wananchi wanaozungukwa na viwanda hivyo kwa Serikali ni kusikilizwa  kwa madhara wanayoyapata na kuacha tabia ya kuvifungia kwa muda mfupi viwanda hivyo baada ya kubainika kuwa vimekiuka kanuni za uhifadhi wa mazingira
Baraza la Uhifadhi wa  Mazingira (NEMC) limekuwa likivifungia viwanda hivyo kwa muda mfupi, jambo ambalo limekemewa na wakazi hao wakitaka adhabu kali zaidi itolewe kwa viwanda husika. 
Zipo baadhi ya kampuni na viwanda nchini ambavyo pamoja na kupewa onyo na mamlaka zinazohusika, bado zimeendelea kuchafua mazingira kwa kutiririsha maji yanayoathiri binadamu na mifugo, jambo ambalo linahatarisha afya za wananchi katika maeneo wanayoishi.
Mmoja wa wakazi wa jiji la Mbeya aliyejitambulisha kwa jina la Gladness Bakari, amesema taka ambazo zinaweza kusababisha matatizo ya afya ni pamoja na za viwandani, taka ngumu kama vifuko ya plastiki, vinyesi na hata vumbi la migodini na kadhalika, huku akisisitiza kuwa athari hizo zinaweza kuwa za kimwili, mikrobiyolojia, biyolojia au kemikali ambazo ni vikolezo vya magonjwa.
Akizungumza Mwanasheria wa NEMC, Heche Suguta, amekiri kuwa baraza hilo limekuwa likipokea malalamiko mengi kutoka kwa wakazi ambao wanavizunguka viwanda hivyo pamoja wakilalamikia vumbi na kelele kuwaathiri kiafya.
Pamoja na hayo amekiri kwamba Baraza lilijulishwa kuwa uchafuzi unaofanywa na baadhi ya viwanda Jijini Dar es Salaam (hakutaja jina) umesababisha watoto kupata mafua yasiyoisha, kukohoa, kuumwa vichwa na Kifua Kikuu (TB), walilalamikia wakati mwingine kushindwa hata kulala kutokana na hali hiyo.
Kiwanda cha MMI Steel kinacholalamikiwa kwa uchafuzi wa mazingira

Viwanda hivyo vimekuwa zikiamriwa kulipa mara moja faini isiyopungua milioni 40 kwa kuvunja kifungu namba 191 cha sheria ya mazingira ya mwaka 2004. Kiwanda cha Saruji Songwe ambacho kiko jirani na uwanja wa ndege Songwe, Mbeya ni moja ya viwanda vinavyolalamikiwa kwa tatizo la vumbi kuathiri wakazi wanaozungukwa na kiwanda hicho.
Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 1992, lilitoa kauli kwamba licha ya sekta ya viwanda kukua na kuwa miongoni mwa sekta mama katika kukuza uchumi na kupunguza tatizo la ajira, ujenzi holela wa viwanda jirani na makazi ya watu ni hatari kwa afya za wananchi.
Mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, Shafii Haruna, anayeishi karibu na moja wapo ya kiwanda kinachofanya uzalishaji wa bidhaa za mafuta ya kupaka na sabuni ameelezea namna anavyonufaika na kiwanda hicho na hatari inayomnyemelea kuwa ni pamoja viwanda hivyo kutiririsha maji machafu katika mifereji inayochezwa  na watoto wadogo ambao hawana uelewa wa madhara ya maji hayo.
Kwa mujibu wa mkazi huyo, wananchi jijini humo wanatakiwa kuhakikisha wanathamini matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya kuni na madhara yanayotokana na viwanda.
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais –  Mazingira, imevitaka viwanda nchini kujenga utaratibu wa kutathmini afya za wananchi ambao ndiyo chimbuko la maendeleo ya taifa lolote duniani.
“Wananchi wabadilishe matumizi ya nishati kwa kutumia kuni na mkaa kwa kuzingatia teknolojia muhimu zilizopo sasa kwamaana watatumia kiasi kidogo cha kuni, viwanda vizingatie uzalishaji bora wa bidhaa na kupunguza uzalishaji joto na kuwa na mifumo mizuri ya maji taka” kilieleza chanzo chetu kutoka katika Ofisi hiyo.
Taarifa kutoka kwenye Ofisi hiyo zinabainisha kuwa, wakati hayo yakitokea bado Serikali ipo kwenye mkakati wa kutengeneza mazingira kwa ajili ya kuwavutia wadau wa maendeleo kwenda kuwekeza kwenye mikoa ya pembezoni wakati hali ilivyo katika miji na majiji bado ikiwa hairidhishi.











Barabara inayolalamikiwa kumwagiwa mabaki ya malighafi zinazozalishwa katika kiwanda  cha kutengeneza Nondo na Mabati cha MMI STEEL cha Jijini Dar es Salaam
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa chini ya sheria ya kimataifa kuhusu Haki za Binadamu, serikali zina wajibu mwingi katika kulinda haki za kuishi za raia yao. 
Azimio la haki za binadamu kote ulimwenguni (Universal Declaration of Human Rights), makubaliano ya Kimataifa Juu Ya Haki Za Kiuchumi na Kijamii Na Kiutamaduni (International Covenant on Economic and Social and Cultural Rights-ICESCR) na Mkataba Juu Ya Haki Za Watoto (Convention on the Rights of the Child -CRC) zote zinaweka haki ya kupata hali nzuri sana ya afya iwezekanayo chini ya mkataba huu wa ICESCR, inajumuisha wajibu wa kuboresha afya ya mazingira, kuwalinda wananchi dhidi ya hatari za kiafya katika mazingira, kuhakikisha mazingira ya kazi yenye afya na kulinda haki ya kupata chakula na maji safi.
Dunia ya leo inakabiliwa na ongezeko la joto duniani, uharibifu wa mazingira na matatizo mengine kama vile machafuko, vita na mauaji ya mtu mmoja mmoja na ya kimbari, ugaidi, uvamizi na ukaliaji wa kimabavu wa nchi moja dhidi ya nyingine, Utengenezaji wa silaha za maangamizi (WMD), nyukilia, za kibaiolojia na nyinginezo. Tatizo kuu linalosababisha haya ni mtu kaacha au kapunguza uhusiano wake wa kiutu na mazingira yake.-FIKRA PEVU

No comments: