.

.
TZ WAKA BLOG TUNAKUTAKIA HERI YA MWAKA MPYA 2016, MWAKA HUU UWE WA BARAKA NA MAFANIKIO KWAKO | KUTANGAZA NA BLOG HII WASILIANA NASI KUPITIA 0716 979 939 AU BARUA PEPE tzwakablog@gmail.com

MSD YATOLEA MAELEZO VIFAA VILIVYOPELEKWA MUHIMBILI



BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza kupeleka vifaa tiba kwenye Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), vifaa ambavyo vimenunuliwa na Ofisi ya Bunge kwa agizo alilotoa Rais Dk. John Magufuli.

Vifaa hivyo vilianza kupelekwa juzi katika Taasisi hiyo ili kukabiliana na uhaba alioubaini Rais Magufuli baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika mapema mwezi huu.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu akizungumzia kuhusu vifaa hivyo  wakati wa usambazaji alisema hivyo vyenye gharama ya sh. milioni 251 ni pamoja na vitanda 300, magodoro 300, viti vya kusukuma (wheel chairs) 30, vitanda vya kubebea wagonjwa (stretchers) 30, mashuka 1,695 na mablanketi 400.

Alisema MSD ilianza kupeleka vifaa hivyo MOI mwishoni mwa wiki na kuwa itaendelea kutoa vifaa hadi wiki hii inayoanza leo.

Fedha hizo zilizotumika kununulia vifaa hivyo zilitokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa wakati akilihutubia bunge mjini Dodoma mwishoni mwa wiki ambapo alilitaka bunge kutumia sh. milioni 15 tu kwa ajili ya kujipongeza na kiasi hicho kilichobaki kitumike kununulia vifaa hivyo.

____
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Agizo alilolitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge zipelekwe Katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda na magodoro ya wagonjwa wanaolala chini limetekelezwa.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema fedha hizo zimefanikisha kupatikana vitanda 300 vya wagonjwa pamoja na magodoro yake, shuka 600, Baiskeli za kubebea wagonjwa na vifaa vingine na kwamba hivyo vyote tayari vimepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Balozi Sefue ameuagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha vitanda vyote vinafungwa kesho jumapili na kwamba atakwenda kuvikagua siku ya jumatatu vikiwa tayari vinatumiwa na wagonjwa waliokua wanakosa vitanda vya kulalia na kulazimika kulala chini.

Wadau mbalimbali walichanga fedha kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge baada ya uzinduzi rasmi wa bunge la 11 lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliagiza fedha hizo zitumiwe kwa kiasi kidogo kisichozidi shilingi milioni 15 na nyingine zipelekwe hospitali ya Muhimbili kutatua tatizo la uhaba wa vitanda.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU,

Novemba 21, 2015.

No comments: