Tamko la kulaani mauaji na matukio ya uvunjifu wa sheria wakati wa kampeni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani huko Tarime
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa sana na vurugu za ushabiki wa kisiasa zilizoanza kujitokeza wakati wa mikutano ya kampeni za vyama vya siasa katika sehemu kadhaa nchini.
Matukio ya uvunjifu wa amani na sheria za nchi ambayo yametangazwa na vyombo vya habari hivi karibuni, ni tofauti na jinsi mikutano mikubwa iliyofanyika kwa amani siku za mwanzo za uzinduzi wa kampeni za vyama na wagombea urais wa vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari inaonyesha kwamba kuna ongezeko la vurugu zinazotokea kutokana na wafuasi wa vyama vya siasa kuingiliana katika mikutano ya kampeni na kusababisha vurugu, ama wafuasi hao kupigana.
Tume imepata taarifa ya kutokea vurugu kama hizo ambazo zimesababisha kifo cha mtu mmoja na watu wengine kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga, uharibifu wa gari la mgombea ubunge wa jimbo la Tarime mjini, Bi. Esther Matiko. Vurugu hizo zilizowahusisha wafuasi wa
vyama vya CCM na CHADEMA zilitokea kijiji cha Mangucha, jimbo la Tarime Vijijini, Septemba 10, 2015.
Pia Tume imesikitishwa na taarifa za vyombo vya habari zinazoelezea vurugu zilizofanyika hivi karibuni wakati wa kampeni zinazoendelea katika baadhi ya maeneo nchini, yakiwemo majimbo ya uchaguzi ya Kyela, Bunda mjini, Dodoma mjini, Dar es Salaam na Zanzibar.
Matukio haya yote ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na yanaenda kinyume na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015 yaliyotiwa saini na vyama vya siasa, ambayo yanavitaka vyama vya siasa na wahusika wote kukataa na kulaani vitendo vya vurugu, fujo, chuki, mafarakano, matumizi ya lugha za matusi na kejeli na kubeba silaha yoyote inayoweza kumdhuru mtu.
Tume inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linatoa ulinzi wakati wa mikusanyiko yote wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Kila ilipopata fursa ya kukumbusha umuhimu wa amani wakati wa uchaguzi, THBUB imefanya hivyo. Tume inapenda tena kuchukua fursa hii kuwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuwaasa wanachama na wafuasi wao kuzingatia amani wakati wote wa mchakato wa kampeni na hadi uchaguzi tarehe 25 Oktoba 2015. Aidha, Tume inawakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuacha kabisa kauli zinazoweza kuchochea wafuasi wao kufanya fujo na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kutokana na hali hiyo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali vitendo hivyo na kutoa rai kama ifuatavyo:
Vyama vya Siasa, wagombea na wafuasi wao wazingatie Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015. Aidha, viongozi wa vyama vya Siasa wawahamasishe na kuwasisitiza wafuasi wao kutanguliza uzalendo zaidi, kuwa na uvumilivu wa kisiasa na umuhimu wa kuilinda amani hasa kipindi hiki cha kampeni na kuelekea upigaji kura.
Wanasiasa wafanye kampeni za kistaarabu na kujiepusha na matamshi au vitendo vitakavyoashiria uvunjifu wa amani vinavyoweza kuwatia hofu wananchi hata washindwe kujitokeza kwenye mikutano ya kampeni.
Wananchi na wafuasi wa vyama kwa ujumla waache jazba na tabia ya kujichukulia sheria mkononi hali inayohatarisha amani na utulivu wa nchi.
Wananchi watambue kuwa wanao wajibu wa kuheshimu uhuru na haki za watu wengine, ikiwemo haki za kuishi na uhuru wa kujumuika na kushiriki katika masuala ya kisiasa.
Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wote watakaobainika kuwa walihusika na mauaji, au uharibifu wa mali na vurugu zilizotokea maeneo mbalimbali.
Mwisho, Tume inatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wale wote waliohusika na matukio ya mauaji, vurugu na uharibifu wa mali wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake.
Imetolewa na:
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Septemba 13, 2015
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
No comments:
Post a Comment